Kisa cha khidhri by dr hud hud
Khidhri
Jina Khidhri hutafsiriwa kwa maana ya “mtu wa kijani” likinasibishwa na neno al-akhdar la Kiarabu lenye maana ya kijani. Katika Hadith, Mtume, swallallahu alayhi wa sallam, anasema, “Mtu huyu alipewa jina hilo la Khidhri kwa sababu alikaa katika nchi kame, isiyoota kitu, tahamaki ikageuka kuwa ya kijani chini yake.”
Rai ya Maulamaa wengi wa Kiislamu ni kwamba Khidhri alikuwa ni Nabii. Qur’an inamzungumzia kama ni mmoja wa waja wa Mwenyezi Mungu waliojaaliwa ilimu, mafuhumu na rehema.
“Basi wakamkuta mja miongoni mwa waja Wetu Tuliyempa Rehema kutoka kwetu na Tuliyemuelimisha ilimu zinazotoka Kwetu.” (18:65)
Kutokana na Hadith za Mtume Muhammad, swallallahu alayhi wa sallam, ndipo tunapofahamu kwa uhakika kuwa mtu huyo mwenye hikima na ilimu aliyeongozana na Musa na kumfunza mambo mbalimbali alikuwa ni al-Khidhri.
Waislamu wanaamini kuwa jamii zote za Mataifa katika vipindi mbalimbali vya historia zilishushiwa nabii mmoja au mwingine kuwaonya juu ya adhabu iliyowasubiri wale waliomuasi Mungu.
Nabii huyo akawaongoza katika njia sahihi ya kumwabudu Mungu. Ni kwa mtazamo huu wa historia ya Manabii ndipo inapoyumkinika kwamba Khidhri alikuwa ni mmoja wa Manabii.
Jina Khidhri au “mtu wa kijani” limenasibishwa na watu wa ilimu na masufi katika vipindi mbalimbali na katika dini mbalimbali. Pasipo kutofautishwa sifa zake, mtu huyu amefungamanishwa na hikima na kazi ya kuelimisha.
Wanahistoria wa leo wanadhani kuwa Al-Khidhri alikuwa ni Kothar wa Khasis, mtu mashuhuri ambaye kwanza kabisa alitajwa katika Fasihi na simulizi za Syria ya Kaskazini.Kothar alikuwa ni mtu wa hikima.
Vyovyote iwavyo ni muhimu kukirejea kisa cha Musa na Khidhri katika Qur’an. Ibn Kathir kasimulia kuwa Musa aliwahi kuulizwa na mtu mmoja, ‘je, kuna mtu katika dunia hii mwenye elimu zaidi yako?”
Musa akasema “hapana!” Akiamini kwamba, kwa vile Mungu alimuwafikia kufanya miujiza na kumpa Taurati basi, moja kwa moja, yeye ndiye aliyekuwa na ilimu zaidi.” Lakini mambo hayakuwa hivyo pale Musa alipokutana na Khidhri.
Mwenyezi Mungu alimwelekeza Musa achukue samaki na pale atakapotoweka samaki huyo ndipo mahali pa kukutana na Al-Khidhri. Musa akatoka kuanza safari ya kumtafuta mja huyo.
Aliandamana na kijana aliyebeba chombo alichokuwemo samaki huyo. Hatimaye wakakutana na Khidhri kama vilevile walivyohakikishiwa na Mwenyezi Mungu.
Kabla ya kusonga mbele na makala haya, twaweza kuona mafunzo katika makutano haya ya Khidhri na Musa. Qur’an 18:66-82 inaanza na hatua ya Musa kukiri kuwa kuna mengi ambayo anaweza kujifunza kwa al-Khidhri huku al-Khidhri akimtahadharisha kuwa hataweza kuvumilia mambo ambayo yeye angeyafanya kwa sababu ya kutojua yalikuwa na maana gani nyuma yake.
Musa akamwambia, “Je, nikufuate ili unifundishe katika ule uwongofu uliofundishwa?” (Al-Khidhri) akasema: “Hakika wewe huwezi kuvumilia kuwa pamoja nami. Na utawezaje kuvumilia yale usiyoyajua hakika yake?” Musa akasema, “Akipenda Mwenyezi Mungu, utaniona mvumilivu wala sitaasi amri yako.” (Al-Khidhri) akasema, “basi kama utanifuata, usiniulize kwa lolote mpaka mimi nianze kukwambia.”(18:66-70)
Kisa cha Musa na Khidhri kinatumika kutuwaidhi kuwa Mwenyezi Mungu ndiye Mwingi wa Hikima. Hapa Mwenyezi Mungu kaikutanisha miamba ya ilimu na hikima ili tupate kujifunza pande zote mbili. Kukutanishwa kwao ni faida kubwa kwetu.
Ni hikima ya Mwenyezi Mungu iliyowakutanisha wawili hao kwa ishara ya samaki. Je, sisi huwa tunazingatia ishara za makutano yetu na wengine ambazo pia zina hekima ya Mwenyezi Mungu nyuma yake?
Hapa Mwenyezi Mungu anatufunza hikima ya kuzingatia ishara na matukio. Maisha yetu yamegubikwa na mitihani ya aina mbalimbali. Kuna majanga, misiba, maradhi na kadhalika.
Wakati mwingine, kwa kushindwa kujua undani wa majanga haya, huwa tunadhani labda tunahilikishwa kwa madhambi yetu, au labda tumemuudhi Mwenyezi Mungu, au tunaweza kulalama, mbona mabalaa yametuandama, mkosi gani huu jamani, au bahati mbaya gani hii! Mkosi gani huu! Na kadhalika.
Lakini kumbe tunapotulizana na kuvuta mazingatio na tafakuri, tunaweza kuuelewa undani wake, tunaweza kupata mafunzo na kuiona hikima ya Mwenyezi Mungu ya kutaka kutusogeza jirani Naye kwa mitihani hiyo, na kisha kutuzawaidia Pepo Yake Tukufu.
Kuiridhia Qadari ya Mwenyezi Mungu hata kama mwanzo twaweza kuhuzunika, kusononeka na kuuliza imekuwaje hili likawa hivi au vile, au tunaweza kuona kama vile tunaelelezwa lakini baadae twaweza kurudisha mazingatio katika Qadari kwamba nyuma yetu kuna Uweza ulio nje ya Udhibiti na Ufahamu wetu.
Matukio yaliyojiri katika safari ya Musa na Khidhri ni salamu muhimu kwetu kwamba kila tukio huwa na Hikima tusioijua undani yake. Ni Waja waliopewa ilimu maalum kama Khidhri walioweza kutangulia kujua hikima ya matukio.
Lakini Mwanafunzi wa Khidhri Musa kama tulivyo sisi alifahamu hikima ya matukio hayo baada ya kutokea tena kwa kufafanuliwa kwake. Lakini angalizo alilolitoa Khidhri kwa Musa ndilo la kujifunza kwamba bila subira ya kuyavumilia tusiyoyajua hakika yake, katu hatuwezi kuiridhia Qadari.
Falsafa kubwa ya Kisa hiki ni kutujengea Uwezo mkubwa wa kuiridhia Qadari. Qadari ni mpango wa maisha wa Mwenyezi Mungu ambao taka tusitake lazima utimie kwetu.
Lakini faraja ni kwamba, Mwenyezi Mungu hututakia kheri katika mpango huo. Hata hivyo, kheri hiyo wakati mwingine hufichikana katika ile ambayo kwetu yaweza kuonekana kama shari. Aya ya Qur’an inautia nguvu ukweli huu kwamba ‘mnaweza kuona jambo fulani ni shari kumbe ndiyo kheri kwenu.’
Kuamini Qadari ni mojawapo ya nguzo sita za Imani. Matatizo yanayotukabili duniani yanaweza kuwa sababu ya maangamizi kwetu kwa kuifumbia macho Qadari, na yanaweza kuwa kheri kwetu kwa kuyanasibisha na qadari.
Mtume swallallahu alayhi wa sallam, anasema, “Ajabu iliyoje ya maisha ya muumini, kwani mambo yote kwake ni kheri, na hii haiwi bali kwa muumini tu. Iinapomtokea jambo baya, yeye hulivumilia kwa subira, na hiyo ndiyo kheri kwake.”
Maoni
Chapisha Maoni